Shule ya Schubart Gymnasium iliyoko Wilaya ya Ulm, Ujerumani ina ushirikiano na Shule ya Msingi Mabonde iliyopo Tukuyu, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya, Tanzania. Katika ushirikiano huo, Shule ya Schubart Gymnasium imeweza kuchangia kununua meza, viti na vifaa mbalimbali vya Shule katika Shule ya Msingi Mabonde. Uhusiano kati ya Shule hizi mbili ulianza mwaka 2009 wakati huo wajumbe wa uhusiano kutoka Tukuyu walipoitembelea Ulm, mmoja wapo akiwa ni mwalimu wa Shule ya msingi Mabonde. Mawasiliano ya kwanza yalifanyika kwa kuandikiana barua. Katika mwaka 2011, wajumbe wa uhusiano kutoka Ulm walitembelea Tukuyu na kuleta zawadi kutoka Shule ya Schubart-Gymnasium na kupeleka katika Shule ya Msingi Mabonde. Uhusiano wa Shule hizi mbili uliimarika zaidi kwa Shule ya Mabonde kutembelewa na Fabian (Mwanafunzi wa Schubart-Gymnasium). Baada ya Fabian kumaliza masomo, alifika Shule ya Mabonde na kufundisha kwa wiki kadhaa. Baadhi ya shughuli zilizopo Shule ya Msingi Mabonde zinafadhiliwa na Shule ya Gymnasium kwa njia mbalimbali.
Mwaka 2013 kikundi cha uhusiano kutoka Tukuyu kilikaribishwa kutembelea Schubart Gymnasium. Ili uhusiano uzidi kuwepo kuna umuhimu kwa wanafunzi wapya kuelimishwa kuhusu uhusiano, na kazi hii inafanywa na Kamati za uhusiano Tukuyu – Ulm.
Shule ya Hans und Sophie Scholl-Gymnasium iliyopo katika Wilaya ya Ulm, Ujerumani, inashirikiana na Shule ya msingi Madaraka iliyopo katika Wilaya ya Rungwe Tanzania. Lengo la ushirikiano huo ni kuwa na mawasiliano kati ya Shule, Walimu na Wanafunzi.
Ushirikiano kati ya Shule ya “Hans und Sophie Scholl”-Gymnasium na Shule ya Msingi Madaraka ulianza mwaka 2011 wakati kikundi cha uhusiano kutoka Ulm kilipotembelea Tukuyu. Tangu hapo, mawasiliano kwa njia ya barua na barua pepe yamekuwa yakifanyika. Mafunzo, Picha na video mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na kubadilishana. Mwaka 2013 kikundi cha wajumbe wa uhusiano kutoka Tukuyu walikaribishwa kutembelea Shule ya “Hans und Sophie Scholl”-Gymnasium. Kwa wakati huu, kuna uhusiano mzuri sana kati ya UNESCO Shuleni “Hans und Sophie Scholl”-Gymnasium na Shule ya msingi Madaraka. Baadhi ya shughuli katika Shule ya Madaraka zinafadhiliwa na shule ya “Hans und Sophie Scholl”-Gymnasium kwa njia mbalimbali.
Wajumbe wa uhusiano kutoka Ulm mwaka 2015 walileta zawadi mbalimbali kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya msingi Madaraka. Shughuli mbalimbali katika Shule ya msingi Madaraka zinafadhiliwa na Uhusiano kati ya Tukuyu na Ulm.